Safari ya kutafuta mafanikio unaweza kuianza nyakati sawa na mwenzako, kinachotufautiana ni bidii na njia ambazo watu wanatumia kuyapata mafanikio. Sasa hapo utofauti unapoanzia ndipo yanapozaliwa Maneno kama “yule tulisoma wote” “wakati anaanza biashara tulianza wote” na mengine mengi.
Hiki ndicho ambacho kinaenda kutokea Kwa vilabu vidogo na vile vya kati nchini Kila nikiitizama Singida Big Stars. Ni miaka michache nyuma hata kwenye ramani ya Soka haikuwepo, hata ilipoanza ramani ya Soka hakuna ambaye alishtuka kuwa Kuna watu tishio wanakuja na wanaenda kufanya yale waliyoyashindwa watu wengi.
Kuna Vilabu toka vimeanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara havijawahi kuonja wala kuhisi harufu ya Mashindano ya kimatifa hapa barani Afrika. Sio Kwa kupenda la hasha ila hata wameshindwa kujitutumua kuweza kufikia huko.
Sasa nikuambie kitu, Singida Big Stars imewachukua Msimu mmoja tu kujiweka kwenye hiyo ramani. Ndio, ni Mwaka mmoja tu. Kama unadhani ni rahisi tu kufanya hivyo basi unashindwa kuheshimu uwekezaji, juhudi na nia ya Singida Big Stars katika kupambana na kujiweka katika ramani.
Labda unaona kawaida ila hapa nitakufanya uone Kwanini nakuambia sio kawaida bali ni matunda ya jitihada za mipango thabiti.
Tuanze ndani ya Uwanja, bila shaka Timu yao inaundwa na wachezaji wenye uzoefu na wenye kiu ya kupambana kuhakikisha wanaitendea haki nembo ya Timu ile.
Kocha Hans der Plujuim ni miongoni mwa makocha bora sana kuwahi kutokea. Unakumbuka enzi zile Klabu ya Yanga inatamba na kampa kampa tena? Hans alikuwa msaada mkubwa sana na kuwafanya Yanga watambe.
Singida Big Stars waliona iko haja ya kuwa na aina Ile ya Mwalimu, amekuja ameikuta Ligi ipo kwenye ushindani mkubwa, lakini ameweza kuwasaidia Singida Kwa Msimu wa kwanza kufanya makubwa na kuwezesha kumaliza Ligi nafasi Nne za juu.
Wachezaji wenye uzoefu na kucheza Mashindano mbalimbali bila shaka wamejaa Singida. Medie Kagere, Paschal Wawa, Deus Kaseke, Amissi Tambwe na wengine wengi wakiwa na uimara na matamanio makubwa ya kuona wanapambana na kufanya vizuri wameweza kufanya hivyo. Hakuna namna ambayo unaweza kupongeza ubora walio nao Singida Big Stars ushindwe kuwapongeza wachezaji ambao wamefanya kazi kubwa ndani ya Msimu mmoja tu.
Huku nje ya Uwanja naamini Kuna watu hawalali kuhakikisha Kuna kila namna ya kuwasaidia Walimu, wachezaji na Benchi la ufundi kufanya Majukumu yao kwa uzuri kabisa. Hawa wanajitajidi kuhakikisha mtu akisikia kuhusu Singida Big Stars, basi atamani kuifahamu zaidi.
Ndivyo ambavyo Taasisi bora za Mpira hufanya duniani, Leo hii Mchezaji akihitajika na Singida Big Stars anajihisi kuheshimika, anajiona amepanda thamani. Unajua Kwa nini? Tayari Kuna Dunia yao Singida Big Stars imejitengenezea, Dunia ambayo watu wanaiona kwa sura tofauti sana.
Watendaji hawalali kuhakikisha hakuna baya linaigusa nembo Ile ya Singida Big Stars. Hii ni kuhakikisha nembo inaendelea kuwa bora na kuwavutia watu pia.
Leo hii Kuna Vilabu bado vinaishi Dunia ya miaka ya 1990, Klabu haina kitengo cha Masoko, haina kitengo imara cha Habari, Klabu haina mfumo mzuri wa Taarifa za ndani ya Klabu. Kwani hamuwaoni Singida Big Stars walivyofanya?
Kwanini nawatumia Singida Big Stars, Kwa sababu ni mfano unaoendana na Timu zingine ndogo. Kama Kuna watu wapo mda mrefu na wameshindwa kufanya namna wakazifungua nembo zao Kwanini nisiwaambie waitumie Singida Big Stars kama mfano unaoendana na wao? Shitukeni.
Leo hii bila shaka, Jezi ya Singida Big Stars imekuwa ni miongoni mwa Jezi zinazovutia na watu hupenda kuzivaa. Unadhani watu wametokea tu kuzipenda kuvaa? Hapana Singida wametumia muda, nguvu na Pesa pia kuhakikisha nembo yao inaeleweka Kwa wateja wao na kuipenda zaidi. Sasa hao wengine wanashindwa kufanya?
Wiki chache tu hapo nyuma Klabu ya US Monastir ya nchini Tunisia ilivyowasili nchini Kwa ajili ya Mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga, Viongozi wa Singida Big Stars wakaiona ni fursa hiyo, haraka sana wakaenda kuingia nao makubaliano ya mahusiano na Klabu hiyo.
Sasa wamepata faida ya kuweza kuweka Kambi nchini Tunisia huku gharama za Hoteli na Viwanja itahusika Klabu ya US Monastir. Hamjaiona hiyo Faida? Kwani vimekuja Vilabu vingapi hapa nchini Vilabu vingine havioni kama kuna umuhimu wa kutanua wigo wa mahusiano?
Utafika wakati kila kitu kitakuwa mseleleko kwa Singida Big Stars na kila mtu atastaajabu namna ambavyo Klabu hii itaweza kuendesha mambo yao. Nyakati hizi ambazo wanajitafuta kuna Mtu hata hajashtuka Bado wakishajipata ndipo tutawakumbuka.
Watumieni kama sehemu ya kujifunza, sio siri ni wamepiga hatua kubwa Kwa namna ambavyo wanaiendesha timu.
Imeandikwa na Kiepo Benedicto.
Singida Big Stars