NAJIVUNIA NA KUFURAHIA MAENDELEO YANGU NDANI YA SINGIDA – GADIEL MICHAEL
Yapo mambo mengi ambayo wadau na mashabiki wetu mngependa kuyafahamu kuhusu wachezaji wetu. Kupitia tovuti yetu hii, mtapata kufahamu mambo yote mazuri kutoka kwa kila mchezaji kupitia mahojiano maalum.
Mchezaji wetu ambaye ni mmoja wa manahodha ndani ya kikosi chetu na nyota mkubwa wa soka la Tanzania, Gadiel Michael, amefunguka mambo kadhaa yanayomhusu ambayo hajawahi kuyasema popote. Fuatilia makala hii maalum ambayo ilifanywa kwa mtindo wa maswali na majibu. —
Safari ya soka na kucheza Ligi Kuu kwa Gadiel Michael ilianzia Azam FC iliyomlea na kumpa mwanga kuonekana zaidi kwa timu nyingine kubwa ambapo alianzia Yanga alikocheza kwa misimu mfululizo kabla ya kuhamia Simba SC.
ILICHUKUA MUDA GANI KUAMUA KUJIUNGA NA SINGIDA?
“Mchezaji anatakiwa kupata nafasi ya kucheza ili aimarike zaidi. Nilichukua uamuzi wa kutua Singida iliponihitaji toka nina mkataba na Simba, lakini viongozi waligoma kunitoa. Mkataba ulivyoisha nikaongea nao na kuwaambia kijana wenu naombeni nisogee (mbele) nikapate changamoto mpya ndio nikaondoka sikutaka kuongeza tena mkataba”. “Licha ya kukosa nafasi, lakini naomba kukiri kwamba nilifanya mazungumzo mapya na viongozi wakitaka kuniongeza mkataba, lakini kwa kuwa nilikuwa nahitaji kupata nafasi ya kucheza niliomba kuondoka. Nashukuru Mungu nilikubaliwa, sasa najivunia maendeleo yangu ndani ya timu hii kwani nacheza”
NANI ALIKUWA ANAMPA MOYO WA KUVUMILIA UKIWA SIMBA?
“John R. Bocco alikuwa mtu wa karibu yangu sana mara nyingi ndio alikuwa ananipa moyo wa kuvumilia kwasababu aliamini siku zote nina kitu licha ya kukosa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba,”. “Aliamini katika uwezo wangu ndani ya kikosi cha Simba, lakini muda ulipofika hakuwa na budi kukubali uamuzi wangu wa kuondoka Simba. “Alikuwa ananiambia kucheza kwangu ni suala la muda. Kauli yake ilikuwa inanipa matumaini na moyo nikiamini ipo siku nitapewa nafasi na kucheza. Sijawahi kukata tamaa kwenye maisha yangu ya soka kwa sababu ndio kazi Mungu amenipa na familia yangu inapata kula kupitia mpira. Hata wao walikuwa sehemu ya kunipa imani.”
SIRI YA UBORA?
“Kitu cha ziada zaidi ni kujitunza, kufanya mazoezi kwa bidii, nidhamu, na kujua nini nimekifuata ndani ya timu, kwa sababu nimetoka kuaminiwa nikaingia timu ambayo sikupata nafasi sasa najitafuta baada ya kupata nafasi,” “Nafasi niliyoipata Singida siwezi kuichezea nitapambana hadi tone la mwisho kuhakikisha nafikia malengo baada ya kushindwa nilikotoka.”
ALIJISIKIAJE KUCHEZA NAFASI YA KIUNGO?
“Kucheza kiungo mkabaji (namba 6) ilikuwa mara ya kwanza katika mechi za ushindani mkubwa, lakini sikucheza tu bali mwalimu aliniandaa vyema kuitumikia namba hiyo siku ya mchezo,” “Haikuwa rahisi nilipewa taarifa kabla na kuandaliwa kuwa kwenye mchezo ule nitacheza nafasi tofauti na niliyozoea. Namshukuru Mungu nilicheza vyema na kuisaidia timu ushindi nyumbani.”
KWANINI SINGIDA IMEKWAMA KIMATAIFA?
“Nadhani kilichotuondoa kwenye mashindano ya kimataifa ukiwa ni msimu wetu wa kwanza kushiriki ni kukosa uzoefu. Ukiachilia mbali kushiriki kwa mara ya kwanza pia timu ina mchanganyiko wa wachezaji. Kuna ambao wana uzoefu na wengine hawana hiyo inaweza kuwa sababu kubwa ya kushindwa kufikia malengo lakini tunaamini tuna nafasi ya kuendelea kujifunza,”
KUAMINIWA KWENYE KIKOSI CHA KWANZA
“Ndani ya Singida kila kitu kipo sawa na ninayafurahikia maisha yangu ya soka. Furaha ya maisha ya soka inakuja pale unapopata nafasi ya kucheza kwa sababu soka ndio maisha yako. Amani na furaha ndani ya timu haijalishi utakuwa wapi kikubwa uwe na furaha na unafanya kazi yako kama inavyotakiwa hiki ndicho nachokifanya ndani ya timu.”
ANAJUTIA CHOCHOTE?
“Katika maisha yangu ya soka kitu ambacho sitakaa nikakisahau ni kuondoka Yanga baada ya kuitumikia kwa miaka miwili na kutua Simba nikiamini nitatimiza malengo yangu,” “Kuondoka Yanga halafu nilipokwenda sikufikia malengo niliyotarajia ni moja ya tukio ambao sitakaa nikalisahau kwani lilinipotezea mwelekeo. Nashukuru nimerudi kwenye mstari na naanza kujitafuta upya.”
Singida Big Stars